1. |
Vinamsabihi, Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na viliomo katika ardhi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
|
2. |
Yeye ndiye aliye watoa walio kufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda na Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwafikia kwa mahali wasipo patazamia, na akatia woga katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!
|
3. |
Na lau kuwa Mwenyezi Mungu asingeli waandikia kutoka, angeli waadhibu katika dunia. Na katika Akhera watapata adhabu ya Moto.
|
4. |
Hayo ni kwa sababu walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
|
5. |
Mtende wowote mlio ukata au mlio uacha unasimama vile vile juu ya mashina yake, basi ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na kwa kuwahizi wapotovu.
|
6. |
Na mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuyakimbilia mbio kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa mamlaka Mitume wake juu ya wowote awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.
|
7. |
Mali aliyo leta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ili yasiwe yakizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
|
8. |
Wapewe mafakiri Wahajiri walio tolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wa kweli.
|
9. |
Na walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda walio hamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyo pewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.
|
10. |
Na walio kuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu walio tutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walio amini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu.
|
11. |
Huwaoni wanao fanya unaafiki wanawaambia ndugu zao walio kufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamt'ii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita lazima tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.
|
12. |
Pindi wakitolewa hawatatoka pamoja nao, na wakipigwa vita hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia basi watageuza migongo; kisha hawatanusuriwa.
|
13. |
Hakika nyinyi ni kitisho zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasio fahamu kitu.
|
14. |
Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipo kuwa katika vijiji vilivyo zatitiwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasio na akili.
|
15. |
Ni kama mfano wa walio kuwa kabla yao hivi karibuni. Walionja uovu wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.
|
16. |
Ni kama mfano wa Shetani anapo mwambia mtu: Kufuru. Na akikufuru humwambia: Mimi si pamoja nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
|
17. |
Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hiyo ndiyo jaza ya madhaalimu.
|
18. |
Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo khabari ya mnayo yatenda.
|
19. |
Wala msiwe kama wale walio msahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wapotovu.
|
20. |
Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.
|
21. |
Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeli uona ukinyenyekea, ukipasuka kwa khofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri.
|
22. |
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyo fichikana na yanayo onekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
|
23. |
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipo kuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anaye fanya analo litaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayo mshirikisha nayo.
|
24. |
Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hikima.
|