1. |
Mbingu itapo chanika,
|
2. |
Na nyota zitapo tawanyika,
|
3. |
Na bahari zitakapo pasuliwa,
|
4. |
Na makaburi yatapo fukuliwa,
|
5. |
Hapo kila nafsi itajua ilicho tanguliza, na ilicho bakisha nyuma.
|
6. |
Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?
|
7. |
Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha,
|
8. |
Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga.
|
9. |
Sivyo hivyo! Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo.
|
10. |
Na hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu,
|
11. |
Waandishi wenye hishima,
|
12. |
Wanayajua mnayo yatenda.
|
13. |
Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema,
|
14. |
Na hakika waovu bila ya shaka watakuwa Motoni;
|
15. |
Wataingia humo Siku ya Malipo.
|
16. |
Na hawatoacha kuwamo humo.
|
17. |
Na nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
|
18. |
Tena nini kitakacho kujuulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
|
19. |
Siku ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu tu.
|