1. |
WANAULIZANA nini?
|
2. |
Ile khabari kuu,
|
3. |
Ambayo kwayo wanakhitalifiana.
|
4. |
La! Karibu watakuja jua.
|
5. |
Tena la! Karibu watakuja jua.
|
6. |
Kwani hatukuifanya ardhi kama tandiko?
|
7. |
Na milima kama vigingi?
|
8. |
Na tukakuumbeni kwa jozi?
|
9. |
Na tukakufanya kulala kwenu ni mapumziko?
|
10. |
Na tukaufanya usiku ni nguo?
|
11. |
Na tukaufanya mchana ni wa kuchumia maisha?
|
12. |
Na tukajenga juu yenu saba zenye nguvu?
|
13. |
Na tukaifanya taa yenye mwanga na joto;
|
14. |
Na tukateremsha maji yanayo anguka kwa kasi kutoka mawinguni,
|
15. |
Ili tutoe kwayo nafaka na mimea,
|
16. |
Na mabustani yenye miti iliyo kamatana.
|
17. |
Hakika siku ya uamuzi imewekewa wakati wake,
|
18. |
Siku litapo pulizwa barugumu, nanyi mtakuja kwa makundi,
|
19. |
Na mbingu zitafunguliwa, ziwe milango,
|
20. |
Na milima itaondolewa na itakuwa kama sarabi.
|
21. |
Hakika Jahannamu inangojea!
|
22. |
Kwa walio asi ndio makaazi yao,
|
23. |
Wakae humo karne baada ya karne,
|
24. |
Hawataonja humo chochote kibaridi wala kinywaji,
|
25. |
Ila maji yamoto sana na usaha,
|
26. |
Ndio jaza muwafaka.
|
27. |
Hakika hao hawakuwa wakitaraji kuwa kuna hisabu.
|
28. |
Na wakikanusha Aya zetu kwa nguvu.
|
29. |
Na kila kitu Sisi tumekidhibiti kwa kukiandika.
|
30. |
Basi onjeni! Nasi hatutakuzidishieni ila adhabu!
|
31. |
Hakika wachamngu wanastahiki kufuzu,
|
32. |
Mabustani na mizabibu,
|
33. |
Na wake walio lingana nao,
|
34. |
Na bilauri zilizo jaa,
|
35. |
Hawatasikia humo upuuzi wala uwongo -
|
36. |
Malipo kutoka kwa Mola wako Mlezi, kipawa cha kutosha.
|
37. |
Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilio baina yao, Arrahman, Mwingi wa rehema; hawamiliki usemi mbele yake!
|
38. |
Siku atakapo simama Roho na Malaika kwa safu. Hawatasema ila Mwingi wa rehema aliye mruhusu, na atasema yaliyo sawa tu.
|
39. |
Hiyo ndiyo Siku ya haki. Basi anaye taka na ashike njia arejee kwa Mola wake Mlezi.
|
40. |
Hakika tumekuhadharisheni adhabu iliyo karibu kufika; Siku ambayo mtu atakapo ona yaliyo tangulizwa na mikono yake; na kafiri atasema: Laiti ningeli kuwa udongo!
|