1. |
Vinamtakasa Mwenyezi Mungu viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
|
2. |
Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyo yatenda?
|
3. |
Yanachukiza vikubwa mno kwa Mwenyezi Mungu kuwa mnasema msiyo yatenda.
|
4. |
Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wanao pigana katika Njia yake kwa safu kama jengo lilio kamatana.
|
5. |
Na Musa alipo waambia watu wake: Enyi watu wangu! Kwa nini mnaniudhi, nanyi mnajua kuwa hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu niliye tumwa kwenu? Walipo potoka, Mwenyezi Mungu aliziachia nyoyo zao zipotoke. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.
|
6. |
Na Isa bin Mariamu alipo sema: Enyi Wana wa Israili! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu, ninaye thibitisha yaliyo kuwa kabla yangu katika Taurati, na mwenye kubashiria kuja Mtume atakaye kuja baada yangu; jina lake ni Ahmad! Lakini alipo waletea hoja zilizo wazi, walisema: Huu ni uchawi ulio dhaahiri!
|
7. |
Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule anaye mzulia Mwenyezi Mungu uwongo, naye anaitwa kwenye Uislamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhaalimu.
|
8. |
Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu atakamilisha nuru yake ijapo kuwa makafiri watachukia.
|
9. |
Yeye ndiye aliye mtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili ipate kuzishinda dini zote, ijapo kuwa washirikina watachukia.
|
10. |
Enyi mlio amini! Nikuonyesheni biashara itakayo kuokoeni na adhabu iliyo chungu?
|
11. |
Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na piganeni Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yenu na nafsi zenu. Haya ni bora kwenu, ikiwa nyinyi mnajua.
|
12. |
Atakusameheni dhambi zenu, na atakutieni katika Mabustani yapitiwayo na mito kati yake, na maskani nzuri nzuri katika Bustani za milele. Huko ndio kufuzu kukubwa.
|
13. |
Na kinginecho mkipendacho, nacho ni nusura itokayo kwa Mwenyezi Mungu, na ushindi ulio karibu! Na wabashirieni Waumini!
|
14. |
Enyi mlio amini! Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu, kama alivyo sema Isa bin Mariamu kuwaambia wanafunzi wake: Nani wasaidizi wangu kwa Mwenyezi Mungu? Wakasema wanafunzi: Sisi ni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu! Basi taifa moja la Wana wa Israili liliamini, na taifa jingine lilikufuru. Basi tukawaunga mkono walio amini dhidi ya maadui zao, wakawa wenye kushinda.
|