(SWAHILI) QURAN |
86 - ATT'AARIQ |
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU. |
1. | Naapa kwa mbingu na Kinacho kuja usiku! |
2. | Na nini kitakacho kujuulisha ni nini hicho Kinacho kuja usiku? |
3. | Ni Nyota yenye mwanga mkali. |
4. | Hapana nafsi ila inayo mwangalizi. |
5. | Hebu naajitazame mwanaadamu ameumbwa kwa kitu gani? |
6. | Ameumbwa kwa maji yatokayo kwa kuchupa, |
7. | Yatokayo baina ya mifupa ya mgongo na mbavu. |
8. | Hakika Yeye ana uweza wa kumrudisha. |
9. | Siku zitakapo dhihirishwa siri. |
10. | Basi hatakuwa na nguvu wala msaidizi. |
11. | Naapa kwa mbingu yenye marejeo! |
12. | Na kwa ardhi inayo pasuka! |
13. | Hakika hii ni kauli ya kupambanua. |
14. | Wala si mzaha. |
15. | Hakika wao wanapanga mpango. |
16. | Na Mimi napanga mpango. |
17. | Basi wape muhula makafiri - wape muhula pole pole. |